MTU asiyefahamika aliyerusha bomu kwa mkono katika mkutano wa kampeni za
uchaguzi wa madiwani wa Chadema katika kata ya Soweto mkoani Arusha,
imebainika aliandaliwa mazingira ya kutoroka ili asikamatwe na mkono wa
sheria.
Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana kuhusu tukio hilo la kigaidi
lililotokea katika mkutano wa siasa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisema polisi walizuiwa
kumfikia mhalifu.
“Mkutano huu ulikuwa na ulinzi wa Polisi wakiwa na magari mawili na
askari walisimama upande wa Kaskazini ya uwanja na mrushaji wa mlipuko
huo alikuwa upande wa Mashariki ya uwanja huo na akarusha kuelekea
Magharibi.
“Jaribio la Polisi kutaka kumfuata aliyerusha mlipuko huo, zilizuiwa na
makundi ya wananchi ambao walianza kushambulia polisi kwa mawe na
kuwazomea na hivyo polisi wakalazimika kujiokoa badala ya kumsaka
mhalifu,” alisema Lukuvi kwa masikitiko.
Lukuvi alitaka kila Mtanzania ajihoji kwa nini wananchi walishambulia na
kuzuia askari kutimiza wajibu wao, badala ya kusaidia wamkamate
mhalifu.
Kwa nini wazuiwe?
Lukuvi alikumbusha kwamba pamoja na umuhimu wa Polisi katika maisha ya
kila Mtanzania, lakini siku za karibuni, kumekuwa na jitihada za
makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu
binafsi kupandikiza chuki kwa raia dhidi ya vijana wa Polisi.
Juhudi hizo kwa mujibu wa Lukuvi, zimesababisha raia wachukie askari,
wasiwaamini, wasitoe ushirikiano ili hatimaye lengo la kuhakikisha Taifa
halitawaliki, litimie.
“Askari hawa ni ambao wanajitolea usiku na mchana, ili Watanzania wenzao
wawe salama. Hawa ni askari ambao wanauawa kila siku na majambazi
wakiwa wanatutetea, hawa ni askari ambao ni watoto wa Taifa hili nao ni
Watanzania wanaofanya kazi za hatari kwa ajili yetu,” alikumbusha.
Kanisani, sasa Chadema
Shambulio hilo la bomu ni la pili katika matukio ya kuvunja amani na
sehemu ya mfululizo wa matukio ya kuvuruga amani nchini ambapo Lukuvi
alisema aina ya urushaji wa bomu hilo, hautofautiani na mbinu
iliyotumika katika shambulio la Mei 5, katika Kanisa Katoliki Parokia ya
Olasiti mkoani humo.
“Shambulio la Soweto limehama kutoka kanisani sasa ni katika mikutano ya
kisiasa. Nia ni ile ile ya kufanya Watanzania wachukiane, wapigane na
Taifa letu liparaganyike,” alisema.
Alituhumu baadhi ya wanasiasa kushiriki mpango wa kuparaganyisha Taifa,
au kuhakikisha nchi haitawaliki, lakini kwa kujua au kutojua wanaendelea
kutoa kauli za chuki.
“Wanadhani wanajiimarisha kisiasa, kumbe wanapanda mbegu ya uharibifu wa
Taifa letu, itakayozaa chuki, vita na majuto makubwa,” alisema Lukuvi.
Dau, vita ya Nduli
Pamoja na jitihada zilizokwishafanywa za kumtafuta mtuhumiwa, ikiwemo ya
Polisi kupata taarifa ya mwonekano wa mtu aliyerusha bomu hilo, Lukuvi
alisema Serikali inatangaza dau la Sh milioni 100, kwa watakaotoa
taarifa za kumpata mhalifu huyo.
Alifafanua, kwamba kila atakayetoa taarifa atapata Sh milioni 10 na hata
wakiongezeka Serikali itaongeza fedha hizo. Aliwahakikisha wenye
taarifa hizo kuwa, watapewa ulinzi na taarifa zao zitakuwa za siri.
Lukuvi pia alitaka Watanzania wa dini zote, makabila yote na vyama
vyote, waungane kukabiliana na adui wa sasa ambaye alisema ni mbaya
kuliko Nduli Idi Amini, aliyeshambulia Kagera ambaye Watanzania
waliungana kukabiliana naye na kumshinda.
Kamati Bunge yakutana
Kutokana na hali hiyo Spika wa Bunge, Anne Makinda, jana aliitisha kikao
cha Kamati ya Uongozi ya Bunge, ili kujadili na kutoa kauli ya Bunge
kuhusu bomu hilo.
Mbali na kuitisha kikao hicho, pia aliruhusu mjadala bajeti ya Serikali
ianze kwa wabunge kutoa maoni yao bila kuwapo Bajeti kivuli ya Kambi
Rasmi ya Upinzani kutokana na uamuzi wa Chadema kuondoa wabunge wake
wote bungeni na kuwapeleka Arusha bila taarifa rasmi kwa Spika.
CCM, Chadema zifutwe
Kabla ya kuruhusu mjadala wa bajeti kuanza, Mbunge wa Chakechake, Musa
Haji Kombo (CUF), aliomba Mwongozo wa Spika akiitaka Serikali kuacha
kutoa taarifa ya bomu hilo la Arusha, badala yake itoe taarifa ya
matukio yote ya kuvunja amani ya kuanzia Zanzibar mpaka Arusha.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliomba Bunge
liahirishe shughuli zake, wajadili tukio hilo na kuongeza kuwa amepitia
katika mitandao ya kijamii na kukuta wafuasi wa CCM na Chadema
wakitupiana mpira.
Machali alipendekeza ikiwezekana vyama hivyo viwili vifutwe na Msajili
kwa kuwa Tanzania ni zaidi ya CCM na Chadema. Mbunge wa Muhambwe, Felix
Mkosamali (NCCR-Mageuzi), aliporuhusiwa kuomba Mwongozo, alitaka
viongozi wazee wasiwaachie vijana mzigo wa nchi isiyo na amani wakati
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwaachia nchi yenye amani.
Alitaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, George Mkuchika
anayeshughulikia Usalama wa Taifa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk Emmanuel Nchimbi, wajiuzulu kwa alichosema ni kushindwa kukamata
wahalifu.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), aliitaka
Serikali itenganishe tukio hilo na siasa na kuongeza kuwa inaonekana
inamjua mtuhumiwa na kuhoji kama inamfahamu, kwa nini iunde kikosi cha
uchunguzi.
Shuhuda asimulia
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Abdallah Alila (40) ameeleza namna
alivyoona mtuhumiwa wa kurusha bomu lililoua watu watatu na kujeruhi 68,
akikimbizwa na watu waliokuwa kwenye mkutano wa Chadema.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Alila ambaye ni mkazi wa
Arusha, alidai kuwa alikuwa pembeni mwa gari la matangazo katika mkutano
huo, kwenye viwanja vya Soweto.
“Wakati viongozi wa Chadema wakimaliza kunadi wagombea niliona kitu kama
mfuko wa nailoni (Rambo) ukirushwa juu na ulipotua kulitokea mlipuko
mkubwa ambao ulitikisa eneo zima,” alisema.
Aliendelea kusema: “Mimi nilianguka kwenye mtaro nikiwa nimeumia
miguuni, nilipoinuka niliona watu wakimkimbiza mtu anayedaiwa kuwa
mhusika aliyerusha mfuko ule wa plastiki uliosababisha mlipuko.
“Nilisikia kelele za watu wakimkimbiza mtu anayedhaniwa kurusha mfuko
huo, lakini kila walipojaribu kumkamata walishindwa na wengine
kuanguka”.
Alisema mtu huyo ambaye ni mwanamume, alikimbilia karibu na hospitali ya
Kaloleni huku sauti kutoka kwa baadhi ya watu zikisema, “Yule! Yule!”
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo la Soweto katika nyumba za AICC, ambaye
hakutaka jina lake liandikwe, alisema baada ya mlipuko, kulikuwa na heka
heka ikiwamo watu kukimbia hali iliyomlazimu kukimbilia ndani kuokoa
maisha ya wanawe.
Marekani yazungumza
Serikali ya Marekani imelaani tukio hilo ikisema: “Tunatoa pole kwa
familia za waliopoteza maisha na waliojeruhiwa katika uhalifu huo
uliopindukia.
Tukio hili la uoga limetokea baada ya lingine la Mei 5 katika Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi mkoani humo, ambapo watu watatu
waliuawa na zaidi ya 60 kujeruhiwa.
“Tunatoa mwito kukamatwa, kushitakiwa na kuhukumiwa kwa wahusika,” amesema Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
Katika taarifa yake jana, Balozi alisema Tanzania inajulikana kuwa nchi
inayothamini tofauti za kitamaduni na kuvumiliana; na kwamba vitendo vya
uhalifu kama hivi, bila kujali vinafanywa na nani vinatishia kuchafua
na kudhalilisha amani na usalama wa nchi hii tukufu.
Alisema msimamo wa Marekani ni kudumisha ushirikiano na Watanzania wote
na kuwataka waendelee kukataa matukio kama haya yanayofanywa na
wanaotaka kuhatarisha maisha ya wananchi wenzao.
Makamu wa Rais Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal amesema Serikali
itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inabaini kiini cha milipuko
inayotokea mara kwa mara jijini Arusha kwani inafanya wakazi kushindwa
kufanya kazi za uzalishaji mali.
Dk Bilal alisema hayo jana alipotembelea majeruhi zaidi ya 63 wa mlipuko
huo. “Tunataka kujua kiini cha milipuko na ikiwezekana kuidhibiti
kabisa kwani inafanya wakazi wa Arusha kushindwa kufanya kazi,” alisema.
Alitembelea majeruhi walioko hospitali za Mount Meru, Selian na
Elizabeth ambapo aliwapa pole na kusema Serikali inaungana na wafiwa
katika kuomboleza.
Mwingine afariki
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Selian, Dk Paul Kisanga alieleza kuwa
watoto wawili ndugu Fatma na Farida Jumanne wamepelekwa hospitali ya Aga
Khan jijini Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi.
Mtoto mwingine Amir Ally (7) alifariki dunia na kufanya idadi ya
marehemu kuwa watatu ambao ni Judith Moshi (25) ambaye ni Katibu wa
Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) kata ya Sokon One, Arusha na
Ramadhan Juma (15) ambao wote walikufa kutokana na mlipuko huo.
“Madaktari wetu na wauguzi walijitahidi kuokoa maisha ya mtoto Amir
lakini bahati mbaya hawakufanikiwa kutokana na madhara aliyopata
kichwani na hivyo kupoteza maisha,” alisema Dk Kisanga.
Daktari huyo aliongeza kuwa kuhusu mtoto Fahad Jamal (7) ambaye yuko
Chumba cha Wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) wanasubiri
kuwasili kwa timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kutokana na hali yake kutoruhusu kusafirishwa kwenda hospitali
nyingine.
Alisema kwa sasa idadi ya majeruhi waliobaki hospitalini hapo ni 37 na
inaweza kuongezeka kutokana na ujio wa madaktari bingwa wanaotarajiwa
kupokea majeruhi kutoka hospitali ya Mount Meru na St Elizabeth.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alitoa pole kwa
viongozi wa Chadema na wanachama wote na akalaani kitendo hicho na
kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara yake itatoa msaada wa ndege
kupeleka majeruhi itakapohitajika.
CCM, Chadema
Wakati polisi ikiwa inaendelea na kazi ya kusaka wahusika waliofanya
kitendo hicho, tukio hilo limegeuzwa la kisiasa kutokana na baadhi ya
vyama vya siasa kunyoosheana vidole. Mwenyekiti wa Chadema , Freeman
Mbowe amedai Chadema wana ushahidi wa kutosha wa watu waliohusika na
tukio hilo.
“Tuna ushahidi wa kutosha wa picha za video na za kawaida kuhusu
waliohusika na tukio hilo la kinyama la kurusha bomu katika mkutano wetu
juzi,” alidai Mbowe.
Alitoa madai hayo jana nje ya Hospitali ya Selian baada ya kutembelea
majeruhi pamoja na kumjulia hali Mbunge wa Arumeru Mashariki ambaye pia
amelazwa hapo baada ya kushambuliwa.
Nassari ambaye alikuwa Meneja Kampeni Kata ya Makuyuni, Monduli
alishambuliwa na kujeruhiwa kichwani na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa
CCM.
Mbowe alidai chama hicho kina ushahidi wa mikanda ya video ambayo
inaonesha aina ya bomu la kutupa na mkono na kwamba aliyerusha ni askari
wa kikosi cha Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU).
Mbowe pia alidai magari mawili ya Polisi aina ya Toyota Land Cruiser
rangi ya bluu likiwa na askari wawili nyuma na gari aina ya Land Rover
TDI yalitumika kufanya shambulio hilo.
Alitamba, kuwa wataanika ushahidi wote kwa umma, hivyo hata kama ukweli
utafichwa, wao watatoa ukweli wa jambo hilo kwa watu pamoja na vyombo
vya sheria na Umoja wa Mataifa (UN).
CCM yajibu
Wakati Chadema ikitoa shutuma dhidi ya Serikali kuhusu mlipuko huo, CCM
pamoja na kulaani mauaji hayo, imejibu na kusema Chadema inastahili
kubeba lawama zote za kupanga mauaji hayo ikilazimisha kujijengea
umaarufu kwa damu ya Watanzania.
Nape aliwaambia waandishi wa habari jana: “Ni vizuri Serikali
ikachunguza suala hilo kwa muda mfupi na kuhakikisha waliohusika
wanapatikana na kuchukua hatua zinazostahili.”
Alisema pamoja na kulaani na kuitaka Serikali kukomesha vitendo hivyo
nchini, ni wakati mwafaka kwa vyama vya siasa kujitazama upya kwani zipo
kila dalili kuwa tukio hilo lilipangwa.
Alisema Mbowe alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akidai kuwa
tukio hilo ni la kupanga. “Inawezekana tukio hilo limepangwa na Chadema
wenyewe,” alisema Nape.
Aliendelea kusema: “CCM tunaendelea kusisitiza na kulaani juhudi za
wenzetu kujaribu kujenga umaarufu wa chama chao juu ya damu za
Watanzania na juhudi hizo zinapaswa kulaaniwa na wazalendo wote wa ndani
na nje ya nchi”.
Alisema CCM pia inalaani kitendo cha viongozi wa Chadema kujaribu
kutumia baadhi ya misiba na majeruhi wa tukio hilo kisiasa na mwisho wa
siku kwenda kuwatelekeza hospitali baadhi yao, baada ya kuwaahidi kubeba
gharama zote za matibabu na maziko.
Alisema kabla ya tukio hilo alikuwa Arusha na kubaini kauli ya Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema kwamba kama hali inaonesha kuwa mbaya, basi
uchaguzi ule hautafanyika.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kwa nini CCM isihusishwe na tukio
hilo, Nape alisema CCM imeongoza nchi kwa muda mrefu bila fujo lakini
kuna kauli za viongozi wa Chadema kuwa nchi hii haitatawalika.
“Kwa nini waliofanya hivyo wasio wale wanaosema nchi hii haitatawalika?”
alihoji Nape. Kambi Wakati huo huo, umati wa wananchi wamekusanyika
katika viwanja vya Soweto, Arusha palipotokea mlipuko huo wakiomboleza
huku wakipiga na kuimba nyimbo.
Maziko ya marehemu wa tukio hilo yanatarajiwa kufanyika baada ya
uchunguzi wa kitaalamu wa madaktari kukamilika na miili itaagwa hapo
kabla ya kusafirishwa kwenda Kilimanjaro (Judith) , Lushoto (Amir) na
Tabora (Juma).
Nassari hospitalini
Akielezea kupigwa kwake, Mbunge Nassari akizungumza na Mbowe na Nyalandu
hospitalini hapo, alisema alikuwa kwenye kata yake ya uchaguzi lakini
ghafla alizingirwa na watu zaidi ya 30.
Alisema katika kundi pia walikuwamo watu watatu wenye asili ya Kisomali
ambao wawili kati yao ni wakazi wa jimbo lake la Arumeru.
“Hivi siasa kwa kweli tunakwenda pabaya maana mtu anashambuliwa bila
sababu, nimeumizwa mimi pamoja na mawakala na viongozi wa Chadema
waliokuwa Makuyuni,” alisema.
Habari hii imeandikwa na Joseph Lugendo na Sifa Lubasi, Dodoma na Veronica Mheta, Arusha.
No comments:
Post a Comment